Mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba wameombwa radhi na kocha Sven Vandenbroek, kufuatia kikosi chake kupoteza alama tatu muhimu dhidi Young Africans, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao pekee la mshambuliaji Bernard Morrison lilitosha kuipa Young Africans ushindi katika mchezo huo, ambao ulishuhudiwa na Rais wa Jamuhuri Ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli, na Rais wa shirikisho la soka barani Afrika CAF Ahmad Ahmad.

Morrison aliwainua mashabiki wa Young Africans katika dakika 44, kwa kupiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa klabu hiyo yenye historia ya kutwaa ubingwa wa Tanzania bara mara nyingi.

Kocha Sven amesema kwa jinsi walivyofanya maandalizi na wachezaji wake, hawakutegemea kupoteza mchezo huo, ambao waliupa uzito mkubwa, kwa kuamini walipaswa kupata alama tatu.

“Kama timu tumeumizwa na matokeo haya kwani hayakuwa matarajio yetu na tulikuja tukiwa na malengo ya kuwapa raha mashabiki ila jambo halikuwezekana,” alisema Sven.

“Ila tumejifunza vitu vingi katika mchezo huu baada ya kupoteza, na tutakwenda kuvitumia katika michezo ijayo.

“Bahati mbaya kwangu kupoteza mchezo wa Dabi dhidi ya Young Aficans, kwani ni rekodi ambayo iliwekwa miaka minne nyuma,” alisema Sven.

Kwa upande wa kocha wa Young Africans, Luc Eymael amesema amefurahi kuvunja rekodi ya miaka minne kwa kuifunga Simba, ambayo makocha wengi wameshindwa.

“Timu yangu ilikuwa bora katika maeneo yote na tulicheza soka safi mkubwa ambao umetufanya kuwamiliki na kuwafunga Simba,” alisema Eymael.

“Niwapongeze wachezaji wangu kwani mambo mengi ya kiufundi ambayo niliwapatia wamekwenda kuyafanyia kazi.

“Kwangu mchezo wa Dabi si suala kubwa mno kwani nimecheza michezo mingi ya aina hii na nina mbinu ya kuwazuia, ndio maana nimeweza kupata nilichokitaka.”

“Malengo makubwa kwa timu yangu ni kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi, kwani nafasi ya ubingwa na alama ambazo tumeachwa ni ngumu kuzifikia na kuwapita vinara,” alisema.

“Niwapongeze mashabiki wa Young Africans ambao walijitokeza kwa wingi uwanjani, kwani huu ushindi ni zawadi kwao ya kuendelea kuwa na furaha,” alisema Eymael.

Kwa ushindi wa jana Jumapili, Young Africans wamefikisha alama 50 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya tatu, wakizidiwa alama moja na Azam FC inayoshika nafasi ya pili ingawa imecheza michezo zaidi.

Mabingwa watetezi, Simba SC wanaendelea kuongoza Ligi Kuu, wakiwa na alama 68 baada ya kucheza michezo 27.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohammed, Lamine Moro, Said Juma ‘Makapu’, Feisal Salum/Kelvin Yondan dk 90+4, Papy Tshishimbi, Haruna Niyonzima, Bernard Morrison/Patrick Sibomana dk 56, Ditram Nchimbi na Balama Mapinduzi/Deus Kaseke dk 86.

Simba: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni/Kennedy Wilson dk 23, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone, Clatous Chama, Meddie Kagere/Hassan Dilunga dk 70, John Bocco na Francis Kahata/Deo Kanda dk 62.

Manara awatuliza Simba SC, akiri Young Africans walistahili ushindi
Kamanda wa Al-Shabaab auawa Somalia