Msanii wa muziki wa bongo fleva, Vanessa Mdee, amevunja ukimya kufuatia deni la muda mrefu la kiasi cha pesa anachokidai kutoka kwa kampuni ya usambazaji wa muziki Afrika Mashariki, iitwayo ‘Mziiki’.
Mdee, amepaza sauti kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, Agosti 25, 2022 kwa kuchapisha ujumbe mfupi aliouelekeza moja kwa moja kwa wamiliki wa kampuni hiyo, kama sehemu ya kuhimiza kulipwa stahiki yake itokanaypo na kazi zake za muziki walizozifanya kwa ushirikiano.
Huku akibainisha kuwepo kwa kutothamiwa tena na Kampuni hiyo licha ya kuonyesha jitihada za dhati za kufuatilia malipo yake kwa namna mbalimbali ikiwamo mifumo ya kisheria, lakini suala lake bado halijazaa mafanikio.
“Jamani pesa ya muziki zinatafutwa kwa shida kweli kweli na wasanii kuanza kubuni mpaka ifikapo kwa wananchi, tafadhali Mziiki nawaomba mnilipe pesa zangu kwa makubaliano tuliyonayo, nimejaribu ‘the professional way’ (njia za kitaaluma) na timu yangu, sasa imefika hatua ya nyie kutokujibu.” ameandika Mdee.
Sakata la madai ya haki za Vanessa, linakuja ikiwa ni takribani miaka miwili imepita tangu nyota huyo alipotangaza rasmi kuachana na muziki na kujielekeza katika shughuli nyingine kutokana na sababu mbali mnali zikiwamo changamoto alizowahi kukutana nazo kwenye tasnia hiyo.
Vanessa Mdee, yuko nchini Marekani yaliko makazi yake kwa sasa, akiwa na mchumba wake mwimbaji na muigizaji maarufu, Rotimi.