Shirikisho la soka barani Asia (AFC), limethibitisha matumizi ya Video Assistant Referee (VAR) katika fainali za mataifa ya bara hilo, zitakazounguruma Falme Za Kiarabu (UAE) mapema mwaka 2019.
Mkutano mkuu wa AFC umekubaliana kwa kauli moja matumizi ya teknolojia hiyo, ambayo ilianza kutumika rasmi kwenye fainali za kombe la mabara mwaka 2017 nchini Urusi na baadae fainali za kombe la dunia 2018.
Tayati katika ligi za Hispania, Italia na Ujerumani tekenolojia hiyo, pia imeanza kutumika na kuleta tija kubwa katika maamuzi yenye utata.
AFC ilijadili suala la teknolojia ya VAR katika mkutano mkuu jana Jumatano na kuhakikishiwa na shirikisho la soka duniani FIFA, juu ya matumizi yake ambayo kwa namna kubwa yamepunguza malalamiko kutoka kwa wachezaji, makocha na mashabiki.
Fainali za mataifa ya Asia zimepanga kuanza Januari 05, na michezo yote katika michuano hiyo, itatumia teknolojia na VAR.
Kwa mara ya kwanza fainali hizo zitashirikisha timu 24, baada ya kufanywa kwa mabadiliko ya mfumo wake kutoka ushiriki wa timu 16.
Timu zilizofuzu kucheza fainali za Asia mwaka 2019 ni wenyeji UAE, Thailand, India na Bahrain (Kundi A).
Kundi B: Australia, Syria, Palestina na Jordan
Kundi C: South Korea, China, Kyrgyzstan na Philippines
Kundi D: Iran, Iraq, Vietnam na Yemen
Kundi E: Saudi Arabia, Qatar, Lebanon na Korea Kaskazini
Kundi F: Japan, Uzbekistan, Oman na Turkmenistan