Meneja wa Liverpool Juergen Klopp ameuponda mfumo wa video assistant referee (VAR), baada ya kikosi chake kulazimisha matokeo ya sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Manchester United, jana Jumapili.

Klopp amesema mfumo huo ambao ulibuniwa kwa ajili ya kumsaidia mwamuzi kujiridhisha baadhi ya matukio yenye utata kwa njia ya Video, haukuleta maana yoyote kwenye mpambano huo, ambao ulishuhudiwa na mashabiki wengi karibu ulimwengu mzima.

Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani amelalamikia tukio la mwamuzi Martin Atkinson, kushindwa kutoa adhabu dhidi ya wapinzani wao, kufuatia faulo aliyofanyiwa mshambuliaji wake Divock Origi, kabla ya Man Utd kupata bao la kuongoza.

Chombo kinachosimamia ligi kuu ya England, kilipitisha kanuni ya kutumika kwa mfumo wa VAR, ili kuondoa utata wa kimaamuzi, ambao misimu miaka ya nyuma yalikua yanaleta rapsha baina ya waamuzi, wachezaji, mameneja na mashabiki.

“Hili ni tatizo, tunapaswa kulijadili,” alisema meneja wa Liverpool akiwa katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo kumalizika. “Nilikuwa na uhakika wa asilimia mia moja (100) VAR ingetumika, bao la wapinzani wetu lingekataliwa.”

“Mwamuzi aliamuru mchezo uendelee, kwa sababu alitambua mfumo wa VAR upo uwanjani, lakini cha kushangaza hakuutumia baada ya malalamiko yaliyojitokeza… hatua hii haileti maana. Lilikua tukio la kutazamwa kupitia VAR, lakini ilishindikana kwa sababu anazozijua mwamuzi.

“Sina hasira kwa jambo hilo, lakini ninazungumza kwa kile nilichokiona na kilivyopaswa kuwa. Nina uhakika mwamuzi Martin Atkinson alipaswa kupuliza kipyenga kama kusingekua na mfumo wa VAR, lakini aliamuru mchezo uendelee.”

Kwa upande wa meneja wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer alipingana na malalamiko yaliyotolewa na Klopp, kwa kusema tukio lililomuhusisha Origi ilikua huruma ya mwamuzi, na kama hakupuliza kipyenga ni sahihi kwa mchezo ulivyoendelea.

“Hakukuwa na nafasi ya kufanya hivyo – hatukua tunacheza mpira wa kikapu. Haikua faulo hata kidogo,” Alisema Solskjaer. “Ninafikiri mwamuzi alifanya kazi yake vizuri. Alitumia weledi wake kuhakikisha hapindishi sheria kwa maslahi ya timu ama mtu fulani, alichezesha vizuri sana.”

Mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford alianza kuiandikia bao timu yake kipindi cha kwanza, lakini Adam Lallana aliisawazishia Liverpool dakika tano kabla ya kipyenga cha mwisho.

Licha ya matokeo ya sare ya bao moja kwa moja, majogo wa jiji (Liverpool) wanaendelea kuongoza msimamo wa ligi ya England, wakifuatiwa na Manchester City kwa tofauti ya alama sita, huku Manchester United wakishika nafasi ya 13.

Afariki dunia akidungwa sindano ya kuongeza makalio
Video: Kwa nini wanaume wagumu kuoa, Je tunahitaji upepo wa Kisulisuli? sababu zatajwa