Meneja mpya wa klabu bingwa barani Ulaya Real Madrid Julen Lopetegui amempongeza beki Raphael Varane kwa kutwaa ubingwa wa dunia, akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa.
Lopetegui amewasilisha pongezi hizo, baada ya kufuatilia kwa ukaribu mchezo wa fainali ulioshuhudia Ufaransa wakiichaka Croatia mabao manne kwa mawili, na kutwaa ubingwa wa dunia kwa mara ya pili baada ya miaka 20.
Meneja huyo ambaye alilazimika kuondolewa kwenye kikosi cha Hispania siku mbili kabla ya kuanza kwa fainali za kombe la dunia, kufuatia kutangazwa kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Real Madrid, amesema Varane anastahili pongezi kwa soka safi alilolionyesha wakati wote wa michuano ya kombe la dunia.
Amesema beki huyo alijituma kwa moyo wote na kufanikiwa kufunga moja ya mabao yaliyoipa ushindi Ufaransa dhidi ya Uruguay waliokubali kufungwa mabao mawili kwa sifuri kwenye mpambano wa robo fainani.
Hata hivyo Lopetegui, amesema ana imani kubwa beki huyo ataendelea kuonyesha uwezo wake wa kupambana atakaporejea klabuni hapo kwa msimu ujao wa ligi.
Wakati huo huo Lopetegui amewapongeza wachezaji wake wengine Luka Modric na Mateo Kovacic, kwa taifa lao la Croatia kuchukua nafasi ya pili kwenye fainali za kombe la dunia.
“Pongezi kwa Raphael Varane, kwa kuonyesha uwezo mkubwa na kufikia lengo la kuwa bingwa wa dunia. Pia nawapongeza Luka Modric na Mateo Kovacic kwa kutoa mchango wao hadi kuiwezesha Croatia kuchukua nafasi ya pili, ”
“Luka Modric na Mateo Kovacic wamefanya kazi kubwa sana, ninaamini hali hiyo itahamia kwenye kikosi cha Real Madrid kwa msimu wa 2018/19, ili tuweze kufikia lengo linalokusudiwa klabuni hapa. Amesema mbadala huyo wa Zinedine Zidane.