Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Zainab Chaula ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ubunifu wa kushona vazi (PPE) kwa ajili ya Wataalamu wa Afya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Hedwiga Swai amesema gharama za kutengeneza vazi moja si kubwa kwani wametumia shilingi 30,000 ukilinganisha na vazi lililothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo moja linagharimu shilingi 350,000.

“ Vazi lililothibitishwa na kupitishwa kutumika na WHO ni shilingi 350,000 hadi shilingi 550,000, inategemea umelinunua kutoka nchi gani, “ amesema Dkt. Swai.

Dkt. Chaula alipotembelea kiwanda kidogo cha kutengeneza mavazi hayo amesema “ Leo nimekuja hapa kuwatia moyo kwa kazi kubwa mnayoifanya. Sisi Kama Serikali tunaichukulia Kama jambo jema hasa kipindi hiki cha mapambano ya COVID-19,” amesema Dkt. Chaula.

Ameiagiza Muhimbili kupeleka vazi Hilo katika mamlaka za kuthibitisha ubora wake ili vazi hilo lianze kutumika rasmi na wataalamu.

Dkt. Swai ameishukuru Serikali kwa kutambua ubunifu wa mavazi hayo na kwamba wataongeza juhudi kutosheleza mahitaji ya Wataalamu.

Amesema ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, imewatia moyo kwani ameona jinsi mafundi wanavyotegeneza vazi hilo kwa ustadi wa hali ya juu na hivyo huwezi kuona tofauti kati ya vazi lililothibitishwa na WHO na vazi lililotengenezwa na MNH.

Rage aungana na Waziri Mwakyembe
Naibu waziri afafanua Barakoa za vitambaa kukinga Corona