Mwanadada Venus Williams ametamba kumaliza mbwembwe na mdogo wake Serena Williams za kuendelea kung’ara kwenye michuano mikubwa duniani ya mchezo wa Tennis pale atakapokutana nae kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali ya US Open.

Venus, amekua hafanyi vizuri katika miaka ya hivi karibuni na anapokutana na ndugu yake husumbuliwa kiushindani na kujikuta akitupwa nje ya michuano ya Grand Slams.

Amesema safari hii amejiandaa kikamilifu kutoa upinzani wa kweli na hadhani kama itakua rahisi kwa ndugu yake kufurukuta na kumshinda kirahisi.

Venus, bado anakumbukia kichapo alichokipokea kwenye michuano ya Wimbledon Open miezi mitatu iliyopita kutoka kwa ndugu yake Serena, katika mchezo wa hatua ya robo fainali na mwishowe alifanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Serena, mwenye umri wa miaka 33, hajawahi kupoteza mchezo wowote tangu alipofanikiwa kutwaa ubingwa wa Wimbeldon Open mwaka huu, hali ambayo inaonyesha ni vipi atakavyokua na mshawasha wa kutotaka rekodi yake ya ushindi kuharibiwa.

Akizungumzia mchezo huo Serena amesema utakua mgumu na wakuvutia lakini suala la ushindi kwake analitanguliza mbele na hatokua na nafasi yoyote zaidi ya kuheshimua anacheza na mtu wa aina gani hii leo.

Amesema anamuheshimu sana Venus mwenye umri wa miaka 35 na alijifunza mambo mengi ya kiufundi kutoka kwake, lakini atakaposimama mbele yake hatokua na la ziada, zaidi ya kutimiza ndoto zake za kusonga mbele na ikiwezekana kutwaa ubingwa wa US Open mwaka huu.

Wawili hao kwa mara ya kwanza walikutana kwenye mzunguuko wa pili wa michuano ya Australia Open mwaka 1998, na Venus alifanikiwa kumshinda mdogo wake kwa seti mbili kwa sifuri ambazo ni 7–6 na 6–1.

Kwa ujumla wamewahi kukutana mara 26 na hii leo itakua ni ya 27, ambapo katika mpambano waliyowahi kucheza siku za nyuma Serena ameibuka mshindi mara 15 na Venus amewahi kumshinda mdogo wake mara 11.

Ahadi Mpya Ya Ukawa, Lowassa Na ‘Kaunt Daun’ Yake
Man Utd Kuikabili Liverpool Bila Michael Carrick