Utoaji wa vibali vipya vya ujenzi wa Vituo vya mafuta na mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya vituo vya mafuta umesitishwa na Serikali kwa muda wa miezi mitatu kuanzia hii leo Novemba 10, 2022.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ametangaza uamuzi huo hii leo Novemba 10, 2022 na kusema umefikiwa ili kutoa nafasi ya ufanyaji wa tathmini juu ya ujenzo holela wa Vituo vya mafuta.
Amesema, “Lengo la kusitisha ni kutoa nafasi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wizara zinazohusika na utoaji wa vibali kufanya tathmini ya kina kuhusu ujenzi wa vituo vya mafuta.”
Waziri Mabula, pia ameagiza kusitishwa kutolewa kwa vibali vipya vya ujenzi vinavyokiuka mipango kabambe ya majiji, manispaa, miji na kusitisha ugawaji wa viwanja kiholela unaosababisha taswira za miji kuharibika.