Klabu ya SImba SC imethibitisha kuachana na Kiungo kutoka nchini Nigeria Victor Akpan, baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa nusu msimu, huku sehemu nyingine ya msimu akitolewa kwa mkopo.
Simba SC methibitisha kuachana na Kiungo huyo kupitia vyanzo vyake vya habari, ikiwa ni sehemu ya kuendelea kutangaza watendaji ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo msimu ujao 2023/24.
Taarifa ya Simba SC imeeleza: “Baada ya kuwa kwenye kikosi chetu kwa msimu mmoja, hatakuwa sehemu ya timu yetu ya msimu ujao.”
Victor Akpan alisajiliwa Simba SC mwishoni mwa msimu wa 2021/22 akitokea Coastal Union ya jijini Tanga, lakini alishindwa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo, na kupelekea kutolewa kwa mkopo Ihefu FC wakati wa dirisha dogo mwanzoni mwa mwaka huu 2023.
Kiungo huyo kabla ya kutangazwa kuachwa Simba SC, aliamini angeweza kurejea klabuni hapo na kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha klabu hiyo chini ya Kocha Mkuu Robertinho, kutokana na kucheza mara kwa mara akiwa Ihefu FC, lakini imekuwa tofauti.
Bado Simba SC inatarajia kutangaza wachezaji wengine ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao 2023/24, na kisha itawatangaza waliosajiliwa kwa msimu huo, ambao wamepania kurejesha heshima ya ubingwa wa Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na kufika Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.