Mshambuliaji wa SSC Napoli Victor Osimhen amevunja ukimya baada ya kubezwa kupitia akaunti ya TikTok ya klabu hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukosa Penati katika mechi ya Serie A dhidi ya Bologna na kuzua gumzo mitandaoni, SSC Napoli ikiambulia suluhu.
Wakala wa supastaa huyo, Roberto Calenda alithibitisha kuwa Osimhen alipanga kuichukulia hatua klabu yake kufuatia kitendo hicho.
Calenda aliandika kupitia akaunti ya X akisema: “Kilichotokea kwenye akaunti ya TikTok ya Napoli haikubaliki. Ukweli ni kwamba imemuathiri mchezaji, wamemuongezea matatizo kwani bado ana mgogoro na waandishi wa habari kuhusu taarifa feki kuhusu yeye. Tunataka haki ifuate mkondo wake.”
Baada ya hapo nyota huyo wa kimataifa wa Nigeria alifunguka akisema: “Kuja katika mji wa Naples mwaka 2020 ulikuwa uamuzi mzuri kwangu. Watu wa SSC Napoli walinionyesha upendo wa hali ya juu, na sitakubali watu kuweka dosari kati yetu. Upendo wa watu wa SSC Napoli umenifanya kucheza kwa bidii kutoka moyoni ndio maana navaa jezi kwa kujivunia.
“Kashfa dhidi ya watu wa SSC Napoli si kweli. Nina marafiki wengi kutoka Naples wamekuwa sehemu ya familia yangu na maisha ya kila siku.
Nawashukuru ndugu zangu kutoka Nigeria kwa sapoti na kutoa sauti kwa ajili ya kuniunga mkono.” Osimhen mwenye umri wa miaka 24, alizungumza kutokana na mashabiki kuijia juu SSC Napoli ilipombeza kupitia video kwa kutumia sauti ya kushangaza.
Na katika mwendelezo wa hilo Mshambuliaji huyo aligoma kupiga penalti dhidi ya Udinese na kuanzia benchi wikiendi iliyopita dhidi ya Lecce katika mechi ya Serie A
Osimhen amekubali sakata hilo kumalizwa huku mtendaji mkuu anayedili na mambo ya mitandao ya kijamii ya klabu, Alessio Fortino akijiuzulu nafasi yake.