Chama cha ADC (Alliance for Democratic Change) kimeunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kuwa hakuna mwanafunzi atakayeendelea na shule baada ya kujifungua.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Queen Kathbet amesema wanaunga mkono kwa dhati kabisa kauli hiyo ya Rais Magufuli, amesema mwanafunzi anapopata mimba kwa bahati mbaya au kwa makusudi na kujifungua achukue jukumu la mama na kumlea mtoto wake kisha baada ya hapo wazazi waangalie namna nyingine ya mwanafunzi huyo kuendelea na masomo yake.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo alipokuwa akizindua Barabara ya Bagamoyo – Msata mkoani Pwani na kusisitiza kwamba katika utawala wake, hakuna mwanafunzi yeyote mwenye mtoto atakayeruhusiwa kurudi shuleni kwa sababu Serikali inatoa elimu bure kwa watoto na si wazazi.
-
Prof. Mbarawa amuweka kitimoto mkandarasi Tabora
-
Video: DataVision, TAFCA kuwakomboa wasanii wa sanaa za mikono
Kauli hiyo ya Rais imeibua hisia tofauti tofauti kwani wapo wanaotaka wanaopata mimba shuleni wapewe fursa ya kuendelea na elimu na wengine wamempongeza Rais wakisema kuzuia kuendelea na masomo katika shule za Serikali kutapunguza mimba za utotoni.
Miongini mwa watu waliozungumzia kauli ya Rais Magufuli ni pamoja na mtaalamu wa saikolojia kutoka Kituo cha Afya ya Akili cha Mehota, Dk Bonaventura Bagile ambaye alisema mwanafunzi aliyewahi kubeba mimba anaporudi shule anajenga picha mbaya kwa wanafunzi wenzake.
Alisema wanafunzi wanafundishwa kutofanya mambo fulani wakiwa shuleni, lakini wakiona mwenzao kafanya mambo hayo na bado amerudi shule, hawatakuwa na nidhamu kwa sheria na kanuni zinazowaongoza.
“Mwanafunzi mzazi akiruhusiwa kurudi shule, itajenga image (taswira) mbaya kwa wenzake kwamba ‘you can do something bad and there are no consequences’ (unaweza kufanya jambo baya na usipate matokeo yoyote),” alisema mtaalamu huyo.