Alikiba, Willy Paul na Ommy Dimpoz wameachia ngoma yao mpya inayoenda kwa jina la ‘Nishikilie’ ni moja ya ngoma kali ambayo imeunganisha pamoja wasanii wakubwa Afrika Mashariki wenye sauti za dhahabu.
Utamu wa ngoma hiyo ni namna ambavyo Will Paul anaanza kuimba, Ommy Dimpoz alivyodakia na kuimba sehemu ndogo ambayo inatamanaisha masikio kuendelea kufurahia sauti yake lakini pia pale ambapo mfalme wa sauti bongo, Alikiba alivyoimba vesi ya mwisho ni ngoma nzuri ambayo itaishi.
Tazama ngoma hapa.
Kumekuwa na namna ambavyo binafsi siungi mkono ya wasanii wengi kutumia maneno ambayo kwa tafsiri ya ndani si rafiki hasa kwa wasikilizaji ambao si watu wazima au watoto kwani yamekuwa ni maneno ambayo yanamong’onyoa maadili ya Tanzania.
Nadhani kuna namna nzuri ya kufanya katika utunzi wa nyimbo za wasanii wetu ambazo zitakuwa za kujenga zaidi na si kubomoa, Ndiyo mapenzi yamekuwa dhima inayotumiwa na wasanii wengi katika utunzi wao, tatizo ni maneno yanayotumiwa kuwasilisha jumbe hizo yamekuwa yakileta gumzo yakisindikizwa na video chafu.
Wapo wasanii wachache ambao wanafanya kazi nzuri ambazo hazileti utata wala matabaka kwa rika zote, naweza kutolea mfano Ali Kiba ambaye amekuwa akifanya vyema sana katika sanaa yake kuhakikisha anawasilisha ujumbe wake kwa namna iliyobora zaidi na amekuwa wakimataifa pia kwa kushinda tuzo mbalimbali.
Nadhani atumike kama mfano mzuri wa kuigwa katika nyanja nzima ya namna bora ya utunzi wa maneno fasaha yasiyoleta utata katika tafsiri lakini pia namna bora ya uwasilishwaji.
Sawa kutakuwa na majibu yatayosema lengo la muziki wetu ni kuufikisha kimataifa, nadhani muziki mzuri ni ule usio na utata usiotengeneza matabaka ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu Tanzania, kwani inawezekana.