Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt. Fredrick Shoo amesema dhambi ya watu wenye nafasi kuwakanyaga wengine inapaswa kufanyiwa toba sana katika taifa.
Askofu Shoo amesema hayo Mei 9, 2019 katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi inayofanyika katika KKKT Usharika wa Moshi mjini.
Amesema kuwa dhambi nyingine kubwa ambayo binadamu anapaswa kuifanyia toba ni ile ya kubaguana, na kama Watanzania tunahitaji taifa lipokee baraka kutoka kwa Mungu, ni vyema wakaacha kufanya hivyo.
Amesema jamii inapaswa kujifunza kupitia kwa Mengi kwa sababu alikuwa na nafasi ya kufanya mambo mengi ikiwemo kununua haki za watu wengine.
“Kama kuna kitu tunaweza kumuenzi (Mengi) ni kuiga roho yake ya upendo, kutokuwabagua watu kutokana na matabaka au kabila, nimemsikia mbunge wetu Freeman Mbowe akisema jambo fulani ambalo wakati mwingine huenda tunaongea kwa ndimi kuteleza, tunaomba sana Mungu atusaidie,” amesema Askofu Shoo.
“Tusibaguane kwa misingi yoyote ile, nimefuatilia malumbano yanayoendelea katika mitandao ya kijamii kati ya watu wa chama kimoja na chama kingine nakuta maneno, hadi najiuliza hivi ni Watanzania wameweza kufika mahali kwa namna hiyo.”
Askofu Shoo amesema mwenyekiti Mengi alithamini sana maneno ya maridhiano kati ya Watanzania wote licha ya tofauti zetu, matajiri, maskini wenye mamlaka wasiokuwa na mamlaka kabila hili na kabila lile.
“Leo bwana mtu anapata vimilioni kadhaa tu anataka atembee juu ya migongo ya watu, anapata ka-cheo sijui ni diwani, mkuu wa mkoa, waziri halafu unaona wenzako si kitu. Acha, acha kiburi namuomba Mungu atujaalie roho hiyo ya unyenyekevu.”
Askofu Shoo amesema wakati mwingine anawachukia watu wanaosema Waafrika wamelaaniwa, akaonya kuwa tabia hiyo siyo njema.
“Mengi alituambia tutafute daima kuufahamu ukweli, ndiyo maana alianzisha IPP Media si kwa sababu tu ya kutangaza biashara zake, bali kwa ajili ya kufungua Waafrika wafahamu ukweli na upate kuwaweka huru,” amesema.
Amesema hivi sasa kumekuwapo na watu wanaopenda kupotosha ukweli hata kama wanaufahamu, lakini hawapo tayari kuusimamia huku akimuomba Mungu awajaalie kukaa katika ukweli ili waweze kusonga mbele.
“Ndugu zangu tukiwa na cheo, tukiwa matajiri, tukiwa na uwezo tuutumie kuwasidia watu wengine tuache ubinafsi, tuache kiburi, tuache kujitutumua hasa kwa viongozi wa umri mdogomdogo, kuna mahali mnafika mnajitutumua kama chatu, acheni, unyenyekevu ndugu zangu (ni muhimiu).”
Amesema baada ya kutokea kwa msiba wa Mengi kuna watu walianza kuweka machapisho katika mitandao ya kijamii na kuanza kuhukumu, akawaonya kuwa walikuwa wakikosea na kuhoji kuwa wao ni kina nani kwani kwa utaratibu wa kanisa mtu akitambua dhambi zake na kutubu anarudishwa kundini. “Mtu akisharudishwa kundini wewe mwanadamu mwenye dhambi kama mimi una nini zaidi ya kusemea hapo acha.”
Aidha, amewataka matajiri kuacha kukumbatia mali zao kwa kuwapa wengine, huku akiwataka watu wanaowatetea wananchi wenye haki na masilahi bungeni kufanya kazi yao ipasavyo. “Huu ukawe ni ujumbe kwetu sote na Mungu atusaidie mkalishike hili, mkaendelee kuiombea familia na yale mazuri mengi tuliyojifunza kwake tukayatende,” amesema Dk Shoo.