Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), limewataka wasanii nchini kusoma alama za nyakati na kufuata sheria na taratibu ili kufanya sanaa yenye tija kwa taifa na kuepuka adhabu zinazoathiri kazi zao.

Katibu Mtendaji wa wa Baraza hilo, Godfrey Mungereza ameiambia Dar24 kwenye mahojiano maalum kuwa wasanii wanapaswa kufahamu kuwa huu ni wakati wa utawala wa sheria na kwamba Serikali na idara zake vinafanya kazi kweli.

“Kama ulikuwa umezoea kuchezacheza na kufanya mambo kiholelaholela, tupo kipindi ambacho serikali inazingatia utawala wa sheria, utawala wa kanuni, utawala wa taratibu zote. Kwa hiyo kama walikuwa wanacheza sio kipindi hiki,” Mungereza aliiambia Dar24.

Aliwataka wasanii kutambua nafasi adhimu waliyonayo katika jamii ya kuelimisha, kuonya na kuburudisha. Aliongeza kuwa wanapokuwa wanaimba nyimbo zao waangalie namna wanavyotumia ‘tafsida’ kufikisha ujumbe bila kukashifu watu binafsi, Serikali au viongozi.

Hivi karibuni, BASATA imemfungia msanii Nay wa Mitego kufanya muziki baada ya kukaidi maagizo ya Baraza hilo kufuatia kufungiwa kwa nyimbo zake mbili (Shika Adabu Yako na Pale Kati Patamu).

Ingawa Nay alidai kuwa tayari amemalizana na Baraza hilo na kwamba wimbo wake unaweza kuchezwa baada ya kuuhariri, BASATA wamekanusha vikali madai ya Nay na kueleza kuwa kifungo chake bado kiko palepale kwakuwa hajakamilisha masharti.

Angalia video hii kupata mengi waliyokanywa na kushauriwa:

Watalaamu Kutoka Japani Waja Kujitolea Nchini
Mchungaji afariki akijaribu kushindana na Yesu kufunga