Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limesema kuwa linalaani nguvu kubwa inayotumiwa na Jeshi la Polisi mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi za viongozi wa chama hicho jambo ambalo wamemtaka Jaji Mkuu kuzisimamia mahakama zitende haki.
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi ambapo amesema kuwa licha ya Desemba, 2018 kumuandikia barua Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma bado kuna ukiukwaji wa haki mahakamani.
Amesema kuwa Februari 18, 2019 wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, baadhi ya wanachama walikamatwa na wengine kupigwa walipojitokeza kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.
“Mahakama ni mhimili unaojitegemea na sehemu huru kila mtu anapaswa kwenda kusikiliza kesi kama polisi wakiendelea kuingilia mhimili huu tutegemee mahakama zetu kugeuka mahakama za kijeshi,” amesema Sosopi.