Bodi ya korosho Tanzania imeongeza vituo vya ugawaji pembejeo ili kuharakisha usambazaji na kuhakikisha kila mkulima anapata pembejeo kwa wakati katika kudhibiti kuenea kwa magonjwa na wadudu wanaoshambulia zao la korosho.
Akitolea ufafanuzi tuhuma za ucheleweshwaji wa madawa na viuatilifu Mwanasheria na Katibu wa Bodi hiyo, Ugumba Kilasa amesema kuwa bado wapo ndani ya wakati kwa kuwa matumizi ya viuatilifu huanza mara tu korosho zinapotoa maua mwezi Juni.
Amesema kuwa kufikia Agosti 20, 2017 usambazaji wa pembejeo kwa wakulima wote kwa msimu mpya utakuwa umekamilika kwani tani zilizobaki kukamilisha usambazaji kwa wakulima wote tayari zimeingia bandarini na zipo katika taratibu za kutolewa ili kusambazwa.
“Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ilitoa uamuzi wa kugawa bure madawa na pembejeo kwa wakulima wa zao la korosho kwa lengo la kumwezesha mkulima na kumjenga kiuchumi ili awe na uwezo wa kujinunua mahitaji hayo kwa misimu inayofuata” amesema Kilasa
Hata hivyo, amewaonya wale wanaotoa maneno ya kuwavunja moyo wakulima wa zao hilo kuhusu kusambazwa kwa madawa na viuatilifu kwambi si huduma ya bure na kusema kwamba serikali imeamua kutoa madawa hayo kwa wakulima bure na kila mtu atapata kulingana na mgawo wa madawa hayo
.