Rais wa China, Xi Jinping amefungua rasmi daraja refu zaidi duniani, ambalo limekuwa likijengwa kwa miaka tisa.
Daraja hilo lina urefu wa 55km (maili 34) na Linaunganisha miji mitatu muhimu kusini mwa China ambayo ni Hong Kong, Macau na Zhuhai.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha BBC, Ujenzi wa daraja hilo umegharimu dola 20 bilioni (£15.3bn).
Ukitumia mwendo wa kawaida wa kutembea wa 5km kwa saa, basi itakuchukua saa 11 kulivuka daraja hilo ukiamua kutembea, magari yataruhusiwa kuanza kulitumia daraja hilo kuanzia Jumatano.
Daraja hilo, ambalo limejengwa kuhimili mitetemeko ya ardhi na vimbunga, limejengwa kwa kutumia tani 400,000 za chuma, chuma zinazotosha kujenga minara 60 sawa na mnara maarufu wa Eiffel jijini Paris.
Takriban 30km ya urefu wake umepitia baharini kwenye mlango wa Mto Pearl ili kuwezesha meli kupita chini ya daraja hilo, kuna sehemu ya urefu wa 6.7km ambapo daraja hilo linaingia chini ya bahari na kupitia kati ya visiwa viwili vya kujengwa na binadamu na hivyo kuwa kama njia ya chini kwa chini baharini.
Zamani, mtu kusafiri kati ya Zhuhai na Hong Kong angechukua saa nne kukamilisha safari hiyo. Lakini sasa daraja hilo litapunguza safari hiyo hilo hadi kuwa dakika 30 pekee.