Kampuni ya DataVision International inayojishughulisha na Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) pamoja na tafiti mbalimbali, imefanikiwa kutoa ajira kwa maelfu ya watanzania kwa kipindi cha miaka 20.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 1998, Geofrey Mwaijonga amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa kuwaandaa vijana kwenye sekta ya mifumo ya Tehama ambao wengi wao hivi sasa wanafanya kazi na makampuni makubwa ya kimataifa ndani na nje ya nchi.
Mwaijonga ameongeza kuwa mbali na ajira za muda mrefu, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa ajira za muda mfupi kwa watu wengi kupitia tafiti ambazo hugusa kila wilaya nchini.
“Lakini katika ajira za muda mfupi, tunajulikana sana kwa kufanya tafiti katika nyanja mbalimbali, za elimu, afya… tukiangalia kwenye kanzi data yetu tumepata kuajiri zaidi ya watu 500. Tuna mawasiliano kila wilaya ya nchi hii, hakuna wilaya ambayo hatujafika kufanya kazi,”amesema Mwaijonga.
Alisema kuwa moja kati ya siri za mafanikio ya kampuni hiyo katika mifumo ya Tehama ni ubunifu unaozingatia mahitaji ya soko na uhalisia wa mazingira.
“Tumekuwa wabunifu na tumejifunza vitu vingi sana. Moja kati ya mafanikio tuliyoyapata ni kuanzisha mifumo. Moja ya mfumo tulionao hivi sasa unaitwa M-Lipa. Huu ni mfumo unaowezesha watu kufanya malipo na kupokea malipo kwa kutumia simu zao za viganjani, kuona rekodi ya miamala yao na hata ku-integrate (kuunganisha) na mifumo ya kihasibu,” alisema.
Mfumo mwingine ulioanzishwa na kampuni hiyo kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu ni ‘TIKITI’. Mfumo huo husaidia katika kufanya tafiti ambapo huwezesha ukusanyaji wa taarifa kwa kutumia simu za viganjani na ‘tablets’.
Aidha, Mwaijonga alizumzungumzia changamoto zinazozikabili nchi za Afrika kuwa ni pamoja na kutokuwa tayari kupokea mabadiliko ya teknolojia kwa haraka na kuyatumia kwa matumizi chanya.
“Wanasema, ‘usipobadilika ukasubiri teknolojia ikubadilishe, utabadilika vibaya sana’. Vibaya ina maana katika mwelekeo hasi,” amesema.