Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amezindua ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita saba itakayojengwa kutoka Pugu mpaka Majohe.
Mjema amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye kiwango cha Changarawe itasaidia pakubwa kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo, huku ikitarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu.
Aidha, amesema kuwa Serikali ya awamu ya Tano inayo ongozwa na Rais Dkt. Magufuli imedhamiria kuwatumikia wananchi na si vinginevyo.
“Leo hii tunazindua ujenzi wa barabara hii, hii inatokana na Serikali kuwajali wananchi wake na kutaka kuwaondolea kero ambazo zimekuwa kikwazo katika kuwaletea maendeleo, ndani ya miezi mitatu barabara hii itakuwa imeshakamilika,”amesema Mjema.
Hata hivyo, amewaasa wananchi waliovamia hifadhi ya barabara kuanza kubomoa nyumba zao wenyewe kwani Serikali haitalipa fidia yeyote kwa atakaebomolewa.