Bingwa wa dunia wa ngumi uzito wa juu ambaye hajawahi kupoteza pambano Deontay Wilder usiku wa kuamkia leo amempiga mpinzani wake Luis Ortiz kwa kumaliza pambano (Knock Out) katika raundi ya 10, Brooklyn nchini Marekani.
Ortiz ambaye alikuwa mbabe kutoka Cuba ambaye hakuwahi kuonja kupigwa kwenye mapambano yake 30 alionesha upinzani mkubwa kiasi cha kutaka kumzimisha Wilder katika raundi ya saba, lakini mambo yalimgeuka.
Mkono mzito wa Wilder ulimzidia Ortiz kwa kuangushwa mara kadhaa kwenye raundi 10 na kumfanya muamuzi kumuokoa kwa kumaliza pambano. Ushindi huo ulimfanya Wilder kuwa mshindi wa mapambano 40 bila kushindwa (40-0).
Baada ya pambano hilo, Wilder alimtumia ujumbe wa tambo bingwa wa masumbwi ya uzito wa juu, Anthony Joshua akimtaka kukubali pambano kati yao akimuonya kuwa yeye ndiye bora zaidi na kwamba anajua anamuogopa.
“Niko tayari kwa ajili ya mtu yoyote. Mimi ndiye ‘mbaya zaidi’ kwenye hii sayari na nimewaonesha usiku huu. Hivi punde kutakuwa na bingwa mmoja, sura moja na jina moja ambalo ni Deontay Wilder. Haijalishi ukubwa wa misuli yao, ni kuhusu Moyo tu,” alisema Wilder.
- Marekani yaingilia mgogoro wa kisiasa Ethiopia
- Pacquiao atosa pambano la promota, ‘ni kama unanitusi’
Anthony Joshua anaendelea na maandalizi ya pambano kati yake na Joseph Parker Machi 31 mwaka huu, lakini amewahi kujibu tambo za Wilder kuwa hakuna anayemuogopa kama anavyodai.
Pambano la Wilder na Joshua ni moja kati ya mapambano yanayosubiriwa kwa hamu zaidi duniani kote.