Dereva Kiongozi wa Treni inayomilikiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), Daniel Majura aliyeendesha treni iliyowasafirisha Diamond Platinumz, timu yake na wasafiri wengine waliosafiri kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, amezungumzia maboresho yaliyofanywa na Serikali na siri ya safari hiyo kuwa bora zaidi.
Majura ameiambia Dar24 Media kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika wakati wa safari hiyo kuwa, Serikali imeboresha usafiri huo kutoka matumizi ya makaa ya mawe hadi matumizi ya ‘electric diesel’, na sasa ni safari ya raha, kiasi kwamba hata madereva wanaendesha wakiwa wamevaa suti kwani hakuna kuchafuka kama zamani.
Aidha, Dereva huyo ameeleza kuwa tofauti na usafiri wa barabarani, usafiri wa treni ni sehemu ya utalii wa ndani na salama; na kwamba abiria wana uwezo wa kupumzika, kufanya sherehe mbalimbali wakati treni hiyo ikiwa inaendelea na safari.
“Haijawahi kutokea, hii ni mara ya kwanza [mtu kukodi mabehewa ya treni]. Diamond amefanya kitu ambacho ni tofauti na amewafungua wengi kwamba kumbe inawezekana. Sasa hivi TRC iko kibiashara, hata wewe ukiwa na shughuli yako unakwenda kuongea na uongozi wanakupa nafasi jinsi ya kufanya,” dereva Majura ameiambia Dar24.
“Wamesafiri na treni wamefanya kama utalii wa ndani, na nilibahatika kufanya naye safari kwenda naye Dodoma [katikati ya safari ya Kigoma] nikaishia Tabora na nimebahatika tena kurudi naye Dodoma. Yaani safari imekuwa ni nzuri na kila unayemuona ana furaha,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Dereva Majura ametatua utata wa kinachoelezwa na wengi kuwa treni haina breki ya karibu au haraka.
“Breki ya treni unaweza kusimama kwa uharaka na jinsi wewe dereva unataka usimame wapi unavyopenda. Kuna kiwango cha breki unaweza kukivuta unavyopenda kwamba nataka nisimame pale unapiga kiwango fulani cha breki. Unataka usimame haraka, kuna emergence break (breki ya dharura), unapiga na unasimama haraka,” alisema.
Katika hatua nyingine, alizungumzia changamoto wanazokutana nazo barabarani, alisema kuwa changamoto kubwa ni wananchi ambao wamekuwa wakikatiza kwenye maeneo ya reli bila kuchukua tahadhari, hivyo kuongeza hatari ya kugongwa na treni.
Aliwasihi wananchi kuhakikisha wanazingatia alama za barabarani na zilizowekwa kwenye maeneo ya treni ili kuhakikisha kuwa wanakuwa salama wakati wote.
Akizungumzia tofauti kati ya udereva wa treni na basi, alisema kuwa kwanza treni haina usukani (steering) na inaenda kwa kufuata njia yake tu. Pia, hakuna mtu yeyote hata fundi mitambo anayeruhusiwa kuiwasha treni isipokuwa dereva tu.
Angalia video hapa upate undani wa mahojiano hayo maalum na anavyoonesha mitambo inayowasha na kuendesha treni: