Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amejibu tetesi zilizosambaa kuwa ana mpango wa kugombea ubunge katika jimbo mojawapo mkoani Mbeya.
Akizungumza na Dar24 ofisini kwake katika mahojiano maalum hivi karibuni, Dkt Tulia alisema kuwa yeye kama raia wa Tanzania ana haki yake kikatiba kugombea lakini bado hajaweka wazi eneo atakalogombea nafasi hiyo.
“Ni haki yangu ya kikatiba kugombea, lakini sijasema bado nitagombea wapi. Na nadhani wakati huo nitakapofanya maamuzi watu watayasikia kwa sababu huwa sio siri. Lakini kwa sasa hivi najaribu kufanya hizo kazi za kijamii lakini sio kwa lengo la kugombea hasa,” Dkt. Tulia aliiambia Dar24.
Alifafanua kuwa kama ni kugombea ubunge, ni jimbo moja linalotakiwa lakini kazi za kijamii anazofanya zinahusisha maeneo yote nchini.
Dkt. Tulia aliteuliwa kuwa Mbunge na baadaye kugombea nafasi ya Unaibu Spika wa Bunge nafasi ambayo alifanikiwa kuipata na anaitumikia hadi leo.