Waziri wa Madini, Dotto Biteko, amewataka wachimbaji madini wote wasiokuwa waaminifu waachane na kazi ya uchimbaji wa madini na badala yake waendelee na kazi zingine kwani wizi wa madini sasa ni zilipendwa.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa zoezi la kukabidhi Mabilioni ya fedha na masanduku mbalimbali ya vito na dhahabu yaliyokabidhiwa na Mkurugenzi wa Makosa ya jinai (DPP) Biswalo Mganga kwa Benki kuu ya Tanzania (BoT).
”Niwaombe wote wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini na wenye roho za wizi, Wizi wa madini sasa ni zilipendwa utakuwa unatafuta vitu viwili tu Jela au umasikini, na sisi tusingependa kuona Mtanzania anafilisika sababu ya hili jambo, Kodi unayolipa ni asilimia 7 pekee,”amesema Biteko
Aidha, zoezi hilo limeshuhudiwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, Waziri wa katiba na sheria, Dkt. Augustine Mahiga, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dotto James, Waziri wa Madini Dotto Biteko na Kamishina wa Tume ya Madini Profesa Mruma.
Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, pesa hizo zilizotaifishwa zitaelekezwa katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa watanzania na amewaomba watanzania wabadilike na kuwa taifa la watu waaminifu.