Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limekamata watuhumiwa wawili wa ujambazi, injini 23 za pikipiki, silaha aina ya Shortgun moja, bastola mbili na risasi tano baada ya majibizano makali katika maeneo ya Kigogo Luhanga na Mabibo mpakani jijini Dar es salaam.
Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dar es salaam na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Lucas Mkondya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa watuhumiwa hao wa ujambazi wamekamatwa katika operesheni kali inayoendelea kufanyika jijini kwa nia ya kuhakikisha hali ya usalama inakuwepo muda wote kwa raia na mali zao.
Aidha, katika hatua nyingine Kamanda Mkondya amewataka wananchi kusherekea sikukuu ya Idd El Fitri kwa amani pia kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pindi wanapohisi kuna dalili za uhalifu kutokea.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limejipanga vyema kuhakikisha ulinzi na usalama unaendelea kuimarika katika sikukuu hii ya Idd El Fitri, pia operesheni bado inaendelea kila kona ya jiji ili kusafisha kila aina ya uhalifu ambao unaweza kusababisha uvunjifu wa amani”amesema Mkondya.