Jeshi La Polisi nchini Tanzania limefafanua juu ya taarifa ambayo imesambaa kwenye mitandao ikimuonyesha moja ya askari wa jeshi hilo kuwa yupo Nairobi nchini Kenya karibu na hospitali aliyolazwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Akitoa taarifa hiyo kupitia Msemaji jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa ameeleza kuwa taarifa hizo zinazosambazwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee si zakweli ni uzushi unaosambazwa kwa lengo la kupotosha umma.
Amesema, kupitia mitandao ya kijamii kulisambaa picha ya Askari wa Jeshi la Polisi akihusishwa na muendelezo wa tukio la kujeruhiwa kwa risasi kwa Lissu ambapo taarifa hiyo ilimtambulisha Askari huyo kuwa ni kachero wa Kitengo cha Interpol na kwamba yupo humo akifuatilia taarifa za Lissu.
Aidha, Jeshi la Polisi limetumia muda huo kuwatahadharisha wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kupotosha umma kwa kutoa taarifa zisizokuwa na ukweli wowote. Amesema yeyote anayesambaza taarifa hizo za upotoshaji anafanya makosa ya jinai hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Amesema kuwa jeshi hilo linakemea vikali kitendo hicho chenye lengo la kumharibia maisha yake Askari huyo, na amewataka wale wote waliohusika kusambaza au kutajwa katika taarifa hizo kuripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya mahojiano.