Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amesema kuwa mafanikio ya majadiliano yaiyopatikana kati ya Wataalamu wa Serikali ya Tanzania na Barrick Gold Mine kuhusu biashara ya madini ya dhahabu yameweka rekodi ya aina yake.
Ameyasema hayo hii leo Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya kukabidhiwa kwa ripoti ya mazungumzo hayo ambapo amesema kuwa hatua hiyo imeweka historia ya aina yake na ya kuigwa.
“Tanzania tumeonyesha mfano mzuri na kuigwa, na kweli tukiamua tunaweza, haya majadiliano hayakuwa kitu kirahisi, mwisho wa siku tumefanikiwa na naamini kuwa nchi nyingine Afrika zitaamua kuja Tanzania kujifunza namna tulivyofanikiwa,”amesema Rais Dkt. Magufuli
Aidha, amesema kuwa kuanzia sasa Tanzania imeweka kiwango kipya kuhusu mikataba ya madini na kwamba kiwango hicho kilichofikiwa Barrick ndicho kitakachotumika katika majadiliano na kampuni zingine za uchimbaji madini.