Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Mazingira, imefanya ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa ukuta wa fukwe ya Ocean Road katika Barabara ya Barack Obama Jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kukagua mradi wa Mabadiliko ya Tabia nchi, unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stanslaus Nyongo (MB) Maswa Mashariki (CCM) amesema kuwa, kamati itaishauri Serikali kutumia vizuri mahusiano ya nchi na wahisani ili kuweza kupata pesa za kusaidia suala zima la kuhimili na kukabiliana na mbadiliko ya tabianchi.
Aidha, Nyogo ameitaka Serikali kuongeza jitihada za kupambana na kukabiliana na athari na hasara zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa elimu ya kulinda mazingira kwa umma.
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo Dkt. Rafael Chegeni, amesema kuwa uharibifu wa mazingira utokanao na ukataji miti ovyo kwa matumizi ya nishati ya mkaa ni mkubwa na ndiyo unaopelekea athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi, na kuongeza kuwa ni bora kuwe na mkakati unaoonekana wa kusaidia upatikani wa haraka wa nishati mbadala.
Hata hivyo, Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) , na kusimamiwa na Shirika lingine la umoja wa mataifa la Huduma kwa Miradi, (UNOPS) ambalo linasimamia miradi yote ya mabadiliko ya tabia nchi duniani.
Mradi huo upo chini ya Uratibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira. na ujenzi huo wa ukuta unafanywa na kampuni ya Dezo Civil Constractions ya jijjini Dar es Salaam.