Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Nchini, Rogers Sianga, amesema kuwa watu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, wameitesa jamii kwa muda mrefu kwa kusambaza madawa hayo ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Ameyasema hayo mapema hii leo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mk0a wa Dar es salaam, pamoja na viongozi wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa Dini.
Amesema kuwa madawa ya kulevya ni hatari sana na yamesababisha madhara makubwa katika jamii pamoja na kusababisha vifo kwa watumiaji wa dawa hizo.
Aidha, ameongeza kuwa baadhi familia watoto wamebebeshwa mizigo ya madawa ya kulevya kwa ajili ya kusafirisha, kitu ambacho kimepelekea kukamatwa kwa vijana hao katika nchi mbali mbali duniani na kupelekea kufungwa.
Hata hivyo, ameongeza kuwa watu wanaojihusisha na biashara hiyo ya madawa ya kulevya, hawastahili huruma hata kidogo kwani wao ndio chanzo cha kuliangamiza taifa hasa kwa vijana.