Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi bilioni 237.8 kugharamia miradi ya maji nchini.
Majaliwa amesema kuwa atahakikisha anafuatilia kwa kina ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya maji ili kuhakikisha kama inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa katika kugharamia miradi hiyo.
Amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Jiji la Mbeya katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini Mbeya akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.
“Nitafuatilia katika maeneo yote nchini ili kujua kama kiasi cha fedha kilichotolewa kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maji iwapo kinalingana na thamani halisi ya miradi husika. Lengo ni kuhakikisha kwamba thamani ya miradi yote inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.”