Katika kuhakikisha wizi wa mitandao unadhibitiwa na kukomeshwa kabisa na kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano yenye kauli mbiu ya “Hapa kazi tu,”
Kampuni ya DataVision International iliyopo Mikocheni Jijini Dar es salaam, imekuja na mfumo mpya utakasaidia kupambana na kudhibiti wizi wa fedha kwa kutumia mitandao katika mabenki Tanzania, mfumo huo utasaidia mabenki yote yaliyojiunga na Umoja Switch hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Prof. Fredrick Mtenzi wakati akizungumza na Dar24 mara baada ya kuwasilisha mada katika Kongamano lililoandaliwa na kampuni hiyo kwa kushirikiana na Umoja Switch ambalo limefanyika Zanzibar mwishoni mwa wiki.
Amesema kuwa kampuni hiyo imejipanga kusaidia taasisi zote za fedha za Serikali na binafsi ambazo zinafanya kazi na Umoja Switch ili ziweze kudhibiti wizi ambao siku zote umekuwa ni tatizo kubwa katika taasisi za kifedha.
Amesema DataVision itatengeneza mfumo ambao utakuwa unakusanya taarifa zote za benki na kuzituma sehemu husika kwa ajili ya kutoa taarifa za wizi uliotokea, ambapo mfumo huo utasaidia kupambana na kudhibiti wizi huo unao ongezeka kadri teknolojia inavyozidi kukua.