Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kuwa Rais wa kwanza wa nje kutembelea Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Amesema kuwa ukiachilia mbali ujirani uliopo baina ya Tanzania na Kenya, pia kuna undugu kwa kuwa tunazungumza lugha moja, kunamuingiliano wa kijamii ikiwemo kuoana na kuwa na utamaduni unaofanana.

“Kufika kwako umeudhihirishia umma wa dunia kuwa sisi ni majirani, na marafiki wa kweli siku zote tutatembea pamoja kamwe tusikubali kulaghaiwa na watu,” amesema Rais Magufuli.

Amesema kuwa kutokana na ushirikiano huo wafanyabiasha wa Kenya na Tanzania wamekuwa wakishirikiana katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kijamii ikiwemo kuwekeza katika nchi zetu.

Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kenya imewekeza miradi 504 yenye thamani ya dola 1.7 biloni ikiwa na idadi ya watu 50,956.

Aidha, katika Sekta ya Utalii, Tanzania ni nchi ya pili kwa watu wake kutembela nchini Kenya ikitanguliwa na nchi ya Marekani ambapo kwa mujibu ya takwimu za bodi ya utalii ya Kenya ya Mwaka 2018 Watanzania 222,216 walitembelea Kenya ambayo ni zaidi ya 10% ya watu wote waliotembelea Kenya.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ameitaja miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa kuwa na ushirikiano wa nchi hizi mbili ikiwemo barabara ya Holili- Arusha hadi Namanga pamoja na maandalizi ya ujenzi wa Barabara kutoka Mombasa hadi Bagamoyo.

Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ipo katika hatua mbalimbali za kujenga meli tano ambapo itaanzisha safari za kutoka Bukoba – Mwanza – Kisumu na Jinja.

Vile vile Rais Dkt. Magufuli ametoa wito kwa wawekezaji kutoka Kenya kuja kuwekeza nchini hapa kwa kuwa milango ipo wazi kwa mwekezaji yeyote na Watanzania waendelee kuwekeza Kenya ili kuendeleza ushirikiano uliopo kwa mustakabari wa maendeleo ya nchi zote mbili.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyata amesema anayofuraha kuwa Rais wa kwanza wa nje kukanyaga ardhi ya Chato.

Ameongeza kwamba uwepo wake Chato Mkoani Geita ni udhibitisho kuwa nchi hizi ni ndugu na wapo kwa ajili ya kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Kenya.

“Hakuna mtu anayeweza kututenganisha kamwe, sisi kama watu wa Afrika Mashariki yatupasa kuhakikisha tunaondoa vikwazo vyote vitakavyozuia kutembeleana, kufanyabiashara pamoja na pengine hata kuoana.”amesema Kenyatta.

Video: Wakili Manyama aibua mapya kuhusu Lissu, 'Spika Ndugai hakukosea'
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 6, 2019