kijana Hamad Awadh mwenye umri wa miaka 28 ambaye alikuwa anatumia mashine ya umeme kupumua mara baada ya mapafu yake kusinyaa na moyo wake kuhama, amefariki dunia jana Oktoba 17, 2019 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mloganzila alikokuwa amelazwa.

Awadh alilazwa Oktoba 4, 2019 kutokana na maradhi ya kushindwa kupumua pamoja na shinikizo la damu ambapo kwa mujibu wa mke wake, Catherine anasema hali ya mume wake ilianza kubadilika jana usiku ambapo aliwekwa chini ya uangalizi wa madaktari hadi kufikia jioni ya jana hali yake haikubadilika ndipo majira ya saa 10 jioni alipoteza maisha.

Aidha, kabla mauti kumfika wadau mbalimbali walijitokeza ili kuweza kumsaidia wakiwemo Tanesco ambao walijitolea kumuwekea umeme kwa ajili ya kusaidia mashine yake anayotumia kupumulia pia ATCL Shirika la Ndege Tanzania lilijitolea kumlipia gharama za usafiri hadi Mumbai, India kwa matibabu zaidi.

Mungu aipumzishe roho ya marehemu kwa amani, aidha Uongozi na wafanyakazi wa Dar24 Media tunatanguliza pole za dhati kabisa kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kwa kuondokewa na mpendwa wao.

Dar24 ilikuwa chombo cha kwanza kilichoenda kumulika hadi nyumbani kwa marehemu enzi za uhai wake na kumuibua kwa kasi iliyozivuta media, mashirika mbalimbali na wadau kulijitokeza kumsaidia hadi pale Mungu alipompenda zaidi.

Pumzika kwa amani Hamad Awadhi. Dar24 Media itaendelea kukuwekea karibu taratibu za mazishi ya awadhi, endelea kufuatilia zaidi.

Mambosasa azungumzia kompyuta za DPP zilizoibwa
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 18, 2019