Kipanya aonesha mchoro wa gari lake kwa mara ya kwanza, asema mawili yajayo ni bora zaidi
Masoud Kipanya, mbunifu na mtangazaji aliyezua gumzo baada ya kuzindua gari la kwanza lililotengenezwa na kampuni yake ya KayPee Motors, ameeleza jinsi alivyofanikisha kazi hiyo pamoja na changamoto zilizopelekea baadhi ya kasoro.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 Media, Kipanya amesema kuwa alianza kuandaa mchoro wenye vipimo maalum vya gari hilo kwa muda mrefu pamoja na mambo mengine yaliyopelekea uundwaji wa gari hilo la umeme.
Mbunifu huyo ambaye kwa mara ya kwanza aliuonesha mchoro wa gari lake katika kipindi cha Dar24 Media, alisema baada ya kulizindua gari hilo alipokea pongezi nyingi zaidi ya kukosolewa lakini vyote anavifanyia kazi kwa usawa.
Akizungumzia changamoto au kasoro ambazo ameziona kwenye gari hilo la kwanza, Kipanya amesema kuwa walipata changamoto zaidi kwenye upakaji rangi, lakini wanatengeneza magari mengine mawili ambayo yatakuwa bora zaidi katika hatua hiyo.
“Bado kuna sehemu unaweza kuangalia ukakuta kuna kasoro kidogo labda za rangi, sehemu kidogo labda imevimba. Lakini kwa ujumla ukiangalia unaona kuna vimakosa. Lakini tulijitahidi sana, kurudia mara nyingi. Kwahiyo, bado kuna hatua ambazo tunaziendea kuhakikisha pasiwe na kasoro,” aliongeza mbunifu huyo.
“Ili ninyi mshangae, ni lazima package ikamilike, na pale ile package haikukamilika. Watu watakapoona gari nyingine hizi mbili zitakapotoka wataona tofauti yake,” Kipanya ameiambia Dar24 Media.
Wiki hii, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) walilikagua gari la Kipanya ambapo walieleza kuwa walitumia viwango vya kimataifa kufanya ukaguzi huo.
Angalia mahojiano kamili ya Kipanya na Dar24 Media, ushuhudie pia mchoro aliouwasilisha: