Taarifa zinaeleza kuwa Klabu ya Young Africans imefungiwa kufanya usajili kwa kipindi cha miaka mitatu, kufuatia kukaidi agizo la kumlipa mshambuliaji wao wa zamani kutoka nchini Burundi Amiss Tambwe.
Mapema hii leo taarifa zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaeleza kuwa Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ ambalo liliagiza mshambuliaji huyo kuliopwa stahiki zake, limefikia maamuzi hayo baada ya kuona muda walioipa Young Africans kulipa deni kupita.
Habari za uhakika kabisa kutoka Zurich nchini Uswisi zinaeleza kuwa Young Africans ilipewa siku 45 kumlipa mshambuliaji wake wa zamani Amissi Tambwe fedha anazodai ambazo alipaswa kulipwa tangu akiwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Young Africans bado hawajalipa hata senti kwa Tambwe ambaye anadai dola 19,000 ambazo ni zaidi ya Shilingi milioni 43.7 na FIFA imeitaka klabu hiyo kuongeza asilimia 5, ikiwa kama ya usumbufu kwa mchezaji huyo.
Hata hivyo alipoulizwa makamu mwenyekiti wa Young Africans Fredick Mwakalebela, amesema suala hilo linapaswa kutolewa majibu na kaimu katibu mkuu Haji Mfikirwa.
Tambwe anadai Young Africans fedha hizo ikiwa za mishahara ya miezi miwili pamoja na kiasi kidogo ambacho hawakumlipa katika fedha yake ya usajili.