Kampuni inayotoa huduma ya mikopo nchini, Kopafasta imezinduliwa rasmi leo Aprili 15, 2019 katika hoteli ya Hyatt Regency Dar es salaam.
Kampuni hiyo inatoa mikopo kwa wanachama waliosajiliwa kupitia miradi mbalimbali kama TACIP na PSG-P inayotekelezwa na kampuni ya DataVision International kwa kushirikiana na Taasisi na Wizara za Serikali.
Lengo kuu la Kopafasta ni kusaidia kurasimisha na kuboresha sekta zisizo rasmi kama Sanaa za Ufundi na Ulinzi binafsi kwa kuanzia, ili kuwasaidia kuwapa mikopo ya fedha, vifaa na vitendea kazi, na kujenga uwezo kupitia mafunzo ya usimamizi wa fedha, biashara na uwekezaji.
Akitoa ufafanuzi wa huduma hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi, Meneja wa Kopafasta, Patrick Kang’ombe amesema sababu ya kutoa huduma ya mikopo kwa makundi hayo kuwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali kumfikia kila mtanzania katika kuboresha na kuweza kujikimu kimaisha.
Amesema licha ya hayo, sekta hizo zimesahaulika na kuchukuliwa kuwa hazikopesheki, kwa maana ya kutokuwa na uwezo wa kuweka dhamana na kutoaminika kupewa mikopo hivyo, Kopafasta wameonyesha kuwa makundi hayo yanaweza kukopesheka.
“Huduma yetu ni tofauti na ya kipekee, kwani tumechagua sekta ambazo zimesahaulika na zimekua zikichukuliwa kuwa hazikopesheki, kwa maana ya kutokuwa na uwezo wa kuweka dhamana na kutoaminika kupewa mikopo..! Hizo zimekua changamoto kubwa kwa sekta zisizo rasmi, na kuzifanya kubaki nje ya mfumo rasmi, pamoja na kwamba zimekua na mchango mkubwa katika pato la Taifa…….”
Amesema wanaamini kuwa, wakiwezesha makundi hayo na kuyaingiza katika sekta rasmi, ni kuunga mkono na kutekeleza sera na jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kama vile kupanua wigo wa walipa kodi na kuongeza pato la Taifa, kukuza ajira, uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, na kuvutia wawekezaji katika Taifa letu.
Aidha, Kang’ombe ametoa wito kwa Serikali kuendelea kusaidia na kuwezesha Miradi inayolenga kutambua na kuratibu wa sekta zisizo rasmi kama TACIP na PSG-P kwa nia ya kurasimisha sekta hizo ili kufanya makundi haya kujitambua, kutambulika na kujithamini ili Kopafasta iendelee kuyakopesha.
“Tungependa pia kutoa wito kwa Serikali kuendelea kusaidia na kuwezesha Miradi inayolenga kutambua na kuratibu wa sekta zisizo rasmi kama TACIP na PSG-P kwa nia ya kurasimisha sekta hizo ili kufanya makundi haya kujitambua , kutambulika na kujithamini ili kopafasta iendelee kuyakopesha.” amesema Kang’ombe .
kopafasta pia imeshirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa huduma hii, ikiwemo huduma ya utumaji na upokeaji wa pesa kwa njia ya simu ya mkononi kupitia mfumo wa M-Lipa. Hii inasaidia kuhakikisha walengwa wa wanapata huduma ya mikopo kwa urahisi na kwa wakati.