Wakati mvutano kati ya Korea Kaskazini na Marekani ukiendelea kuota mizizi, ambapo Marekani imetoa onyo la mwisho kwa nchi hiyo na kueleza kuwa wakati wa kuivumilia Korea umekwisha, Korea Kaskazini imesema iko tayari kwa vita na Marekani.
Akizungumza katika Umoja wa Mataifa, Balozi Kim In-ryong amesema mwenendo wa Marekani kutumia ubabe kuzivamia nchi huru na baadaye kudai inachangia katika kulinda amani ya dunia ni kukosa uwajibikaji na kamwe hawatakubali itokee katika nchi yao.
Hivyo, Balozi Kim In-ryong amesisitiza kuwa Korea Kaskazini iko tayari kwa vita na Marekani.
Korea Kaskazini ambayo hujulikana pia kama Jamhuri wa Kidemokrasia ya Watu wa Korea ilizidisha mvutano wa kikanda kwa kufanya jaribio jingine la kurusha kombora ambalo lilishindwa Jumapili. Wanadiplomasia kadhaa wa nchi hiyo wamesema nchi yao itaendelea kufanya majaribio mengine kila wiki, kila mwezi na kila mwaka.