Mbunge wa Kahama Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mfanyabiashara maarufu nchini, Jumanne Kishimba amesema kuwa amefurahishwa na hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kukutana na wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na Dar24Media mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, ambapo amesema kuwa hatua hiyo ni nzuri na inaleta faraja kubwa kwa wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wadogo wa madini.
Amesema kuwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini wana imani kubwa na rais Magufuli kwani amekuwa ni msikivu na mwenye huruma, hivyo anaimani ataweza kutatua kero zinazo wakabili wachimbaji hao wa madini.
“Kwa hatua hii ya Rais Magufuli ni hatua nzuri sana, kwani tumezungumza na kuwasilisha mapendekezo yetu kwake, tumejadili pamoja na tunaimani yatafanyiwa kazi,”amesema Kishimba