Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema amesema kuwa suala la kutekwa kwa bilionea, Mohamed Dewji si la kunyamaziwa kwani linapaswa kupigiwa kelele kila sehemu.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa kama vyombo vya dola vimeshindwa kulipatia ufumbuzi si vibaya kuomba msaada wa wachunguzi waliobobea kutoka Marekani au Uingereza.
Amesema kuwa kadri muda unavyozidi kwenda hali ya utekaji inazidi kuongezeka, akitolea mfano wa baadhi ya watu ambao inasemekana wametekwa na wengine waliopotea katika mazingira ya kutatanisha.
“Haiwezekani bilionea kama Mohamed Dewji ametekwa mpaka leo hakuna taarifa za kueleweka, yule ni mtu muhimu sana kwa uchumi wa taifa hili, ni lazima serikali ilete wachunguzi wa kimataifa ili tuweze kumpata haraka zaidi,”amesema Lema