Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya  Chama Cha Mapinduzi, Nape Nnauye ametumia dakika takribani 10 kumshambulia mgombea urais kwa kiketi ya Chadema, Edward Lowassa aliyewahi kuwa kada wa chama hicho.

Nape alirusha makombora yake kwa Lowassa jana alipopewa nafasi ya kumnadi mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli katika viwanja vya Samora, mjini Iringa.

Alisema Lowassa ni mwizi na fisadi na kwamba hakuna sehemu ambayo alipewa kufanya kazi katika ngazi za CCM na serikali bila kuiba.

Nape alidai kuwa Lowassa alishindwa kuendelea kukaa katika Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa hawezi kufugika, “Lowassa ni Kunguru hafukigi”.

Katika hatua nyingine, Nape alidai kuwa Lowassa aliwanunua viongozi wa ngazi za juu wa Ukawa na Chadema ili apate nafasi ya kugombea kupitia Chadema ambayo awali ilikuwa ikimuita fisadi. Katika maelezo yake, alisema mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ni miongoni mwa walionunuliwa na Lowassa kwa shilingi milioni 340.

Nape amekuwa akirusha makombora kwa Lowassa tangu alipotangaza uamuzi wake wa kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema. Aliwahi kusema kuwa amekuwa akipambana na Lowassa kwa kipindi cha miaka 12 ndani ya CCM na kwamba ‘muziki’ wake anaufahamu.


Hata hivyo, tangu alipoanza kampeni zake, Lowassa amekuwa kimya bila kurudisha mashambulizi dhidi ya Nape na viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi.

Bila shaka Lowassa atakuwa amemsikia tena Nape Nnauye aliyetumia muda mrefu zaidi kumshambulia  ingawa wakati akiyasema hayo mgombea huyo wa Chadema alikuwa jijini Tanga akifanya mkutano mkubwa uliolazimika kukatishwa kutokana na mafuriko ya wananchi kuzidia eneo la mkutano.

Hata hivyo Nape jana aliwahimiza wakazi wa Iringa kujitokeza kupiga kura ili kuzuia mafuriko [ya Lowassa] kwa kidole.

Je, ukimya wa Lowassa ni busara au kutokuwa na uwezo wa kujibu mashambulizi hayo?

Lukaku Atuma Salamu Anfield
Magufuli Awanyooshea Kidole Wawekezaji Iringa