Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), Dkt. Charles Msonde amesema kuwa njia pekee ya kufaulu mitihani ni kufanya maandalizi mazuri.
Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na Dar24 Media, ambapo amewataka wanafunzi wote kuacha mara moja kufanya udanganyifu katika mitihani.
Amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wanafunzi ambao wamekuwa wakifanya udanganyifu wakati wa mitihani wakiwa na lengo la kutaka kufaulu.
“Nataka niwaase wanafunzi wenye tabia kama hizi waache mara moja, kwani sisi tuna mbinu nyingi sana za kuwabaini, na pindi tunapo wabaini sheria inachukua mkondo wake,”amesema Dkt. Msonde
Hata hivyo, Dkt. Msonde amewapongeza walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya kwani mpaka sasa ufaulu umeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.