Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi Wazara wa Elimu Sayansi na Telnolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda mkoani Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha shule tisa za mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.

Majaliwa ameziagiza halmashauri nchini kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha wanawasimamia vizuri walimu jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na hatimaye kupata matokeo mazuri.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi na wananchi wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo ya Mpanda kwa ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Kwa mujibu wa matokeo hayo kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa zinatoka katika Mkoa wa Mtwara na moja Tanga. Shule za Mtwara zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukodoka  huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.

Majaliwa amesisitiza kuwa viongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini hadi shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana zitoke huko.

Pia, amewataka wasimamie vizuri mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee kupata matokeo mazuri zaidi.

 

Video: 'Rukwa hakuna njaa' - RC
China Wavuruga Harakati Za FC Barcelona