Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maandalizi ya sherehe za miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yanayoendelea katika Uwanja wa Jamuhuri mjini Dodoma.
Majaliwa amesema hayo leo Aprili 24, 2018 mara baada ya kukagua maandalizi hayo yanayofanyika kwenye Uwanja wa Jamuhuri mjini Dodoma, ambapo amesema maandalizi yanaendelea vizuri.
Amejionea maonesho mbalimbali yakiwemo ya kikundi cha halaiki ambacho kinaundwa na wanafunzi 2,000 kutoka Manispaa ya Dodoma pamoja na maonyesho ya kujihami na maadui yaliyooneshwa na Jeshi la Magereza.
“Nimeridhika na kazi ambayo mmeifanya, nawaruhusu muendelee kushirikiana katika kukamilisha maeneo ambayo yamesalia na kuanzia kesho tujiandae kuwapokea wageni kutoka maeneo mbalimbali.”
Alhamisi ya Aprili 26, 2018 Watanzania wanatarajia kuadhimisha miaka 54 ya Muungano tangu Tanganyika ilipoungana na Zanzibar, chini ya waasisi wake Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume.