Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kulifanyia mapitio Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na iwapo hatoridhika na utendaji wake alivunje.
“Ninamuagiza Waziri mwenye dhamana kufanya mapitio na kutathmnini upya utendaji kazi wa Baraza la Michezo Tanzania juu ya usimamizi wake wa michezo nchini na kama hataridhika, anayo mamlaka ya kulivunja Baraza hilo.”
Majaliwa ametoa agizo hilo Julai 5, 2017 katika hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge mjini Dodoma, ambapo amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali maslahi ya Taifa.
“Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo.”
Aidha, Majaliwa ameipongeza timu ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki na kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika.
“Msisitizo wangu kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni kuendelea kuwatunza vijana hao, na kusimamia vilabu vya michezo nchini kuwekeza kwenye soka la vijana ili tujenge timu imara kwa miaka michache ijayo.”
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana nchini.
“Wiki iliyopita, mkoani Mwanza yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA. Wananchi wa Mwanza na Watanzania kwa ujumla wamejionea uwezo wa kimichezo, vipaji na hamasakubwa iliyopo miongoni mwa vijana wetu kutumia vipaji vyao. “
Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa michezo kama somo. “Maelekezo yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na shule angalau mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za kufundisha michezo.”
Majaliwa pia amempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuunga mkono jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya kujenga uwanja mkubwa wa michezo mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki kama vile Morocco ambao wanajenga uwanja huo.