Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha TPC kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro kufanya kazi kwa bidii na kujituma na kuhakikisha wanaongeza tija katika uzalishaji wao.
“Msisitizo wa Serikali ni kuwasihi Watanzania tubadilike, tuchape kazi ili tuweze kuongeza tija mahali pa kazi,” alisema Waziri Mkuu.
Majaliwa amesema hayo wakati alipotembelea na kukagua baadhi ya miundombinu ya kiwanda hicho pamoja na mashamba ambapo wafanyakazi wameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuondoa makato ya kodi kwenye bonasi na muda wa ziada kazini wanaolipwa na kiwanda hicho.
Aidha, Majaliwa ameelezwa kwamba hivi sasa msimu wa uzalishaji umefungwa na kiwanda kinafanyiwa matengenezo ambapo alishuhudia baadhi ya mitambo ikiwa imefunguliwa na kufanyiwa ukarabati.
Pia, ameonyeshwa mtambo wa kuzalisha umeme wa kiwanda hicho (boiler) ambao unatumia mabaki ya miwa yaliyokwisha kamuliwa juisi (bagasse) ambayo huchomwa na kuchemsha maji ili kupata mvuke unaosukuma jenereta.
Akitoa taarifa hiyo Meneja wa Kiwanda, Pascal Petiot amesema kiwanda hicho kimefungwa kwa zaidi ya wiki sita ili kujiandaa na msimu ujao wa uzalishaji ambao uko karibuni kuanza.
“Hivi sasa ni kipindi cha mvua, tumefunga msimu wa uzalishaji na tunaendelea na ukarabati wa mitambo ili kujiandaa na msimu ujao. Kila mwaka ni lazima tufunge msimu kwa kipindi kifupi, ili kufanya ukarabati kama huu,” amesema.
Akizungumzia uzalishaji, Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Robert Baissac amesema uzalishaji wa sukari kwenye kiwanda hicho umepanda kwa asilimia zaidi ya 200 tangu wachukue kiwanda hicho mwaka 2000.
Amesema wakati wanaanza, kiwanda kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 36,000 kwa mwaka na wakati wanakinunua walitakiwa kuongeza uzalishaji kwa asilimia 100 kwa kufikisha tani 72,000 za sukari. “Tuliweza kuvuka lengo hilo tangu mwaka 2007 na hivi sasa tumeweza kuzalisha tani 111,800 katika msimu uliopita,” alisema.
“Tunatumia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na majaribio hapa hapa kiwandani. Tunatumia mbolea na njia za umwagiliaji ili kuhakikisha hadhi ya miwa yetu ni ya kuridhisha, na inayoweza kutupatia kiwango kikubwa cha sukari,” alisema.