Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Januari Makamba ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ili kuongeza tija na kutekeleza kwa vitendo dhana ya Ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Ameyasema hayo mapema hii leo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira na uharakishaji wa miradi ya maendeleo na uwekezaji hasa ujenzi wa viwanda kama azma ya Rais Dkt. John Magufuli inavyoelekeza.
“Utendaji wa NEMC umekuwa ukilegalega sana na umekuwa hauridhishi na kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuhusu ucheleweshaji na urasimu usiokuwa wa lazima katika mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira (EIA)” Alisisitiza Mhe. Makamba
Amesema kuwa ametengua uteuzi wa wajumbe wote saba wa Bodi ya NEMC ili baadaye ateue wajumbe wapya ambao wataendana na kasi na ari ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuelekea uchumi wa Viwanda, ambapo Mwenyekiti wa Bodi ambaye mamlaka yake ya uteuzi ni wa Rais ataendelea kuwepo hadi Rais atakapoteua mwingine.
Vile vile Makamba amesema kuwa changamoto nyingine zilizobainika ni kuwaelekeza wawekezaji kwa makampuni ya kufanya Tathmini ya athari za mazingira ambayo yanamilikiwa au yenye ubia na watumishi wa NEMC, bila kujali mgongano wa kimaslahi jambo ambalo haliruhusiwi katika utumishi wa umma.
Aidha, Jambo jingine ni kuwarundikia maandiko ya miradi ya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) watumishi wachache wakati wengine hawana kazi ili waelekeze miradi hiyo katika makampuni ambayo baadaye huwapatia malipo yasiyo halali.
-
Video: Uongozi NHC wamgusa Waziri Mkuu, atoa pongezi kwa utendaji wao
-
Kigwangalla aagiza kuboresha huduma za afya Wilaya ya Tunduru
-
Waziri Lukuvi abanwa, akesha ofisini kwake
Hata hivyo, ameongeza kuwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC ni muhimu katika kuhakikisha ustawi wa mazingira na mustakabili wa maendeleo endelevu ya nchi inapoelekea kuwa Taifa la uchumi wa viwanda lazima usimamizi wa mazingira uwe thabiti.