Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekabidhiwa ekari 1500 na Mkurugenzi wa Azimio Housing Estate, Mohamed Iqbal kwa ajili ya viwanda vidogo vigogo.
Makonda amekabidhiwa neno hilo mapema leo Februari 21, 2017 ambapo ameeleza kuwa dhamira ya Rais Magufuli ya viwanda inabidi itafsiriwe kwa vitendo, hivyo eneo hilo litatumika kwa ajili ya ufugaji, kilimo, usindikaji, utengenezaji wa sabuni na eneo hilo litatumika na wilaya zote.
Amesema mkoa wa Dar es Salaam unajengwa na wana Dar es Salaam wenyewe hivyo kama kuna watu wanataka kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya Dar es Salaam wafanye hivyo.
Aidha, Makonda amesisitiza kuwa wanaojitolea katika maendeleo ya Dar es salaam wasije wakatumia misaada hiyo kama kichaka cha kujifichia wakifanya maovu yao, kwani bado atawashughulikia kama wakikiuka taratibu na sheria za nchi.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo eneo la Kisarawe II wilaya ya Kigamboni Mkurugenzi huyo amesema wameamua kumkabidhi eneo hilo ili kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli za kuijenga Tanzania ya viwanda na kuwakomboa wananchi wenye uchumi wa kati.