Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa taarifa ya uchunguzi kuhusu biashara ya dawa za kulevya jiji la Dar es salaam na kuwataja watu aliowaita watuhumiwa wa biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Februari 2, 2017, Makonda amewataja vigogo na mastaa wanaotuhumiwa kutumia madawa ya kulevya wakiwemo Askari Polisi 9 wanaotuhumiwa kuhusika na biashara hiyo. Wengine wanaotuhumiwa kutumiwa dawa za kulevya ni mastaa wa filamu na muziki na wametakiwa kuripoti kesho kituo cha Polisi Central.
“Kuna maeneo watu wanatuambia madawa ya kulevya wanayapata sehemu hizo, wamiliki wake kesho niwakute polisi, wasipokuja nitawafuata … kama unajua una eneo unafanya biashara za dawa za kulevya Dar es salaam natoa siku 7 biashara hii iishe, operesheni hii naiongoza mwenyewe. Kama Kamishna Sirro na timu yake watashindwa kutokomeza dawa za kulevya Dar es salaam maana yake wamekosa sifa za kuendelea kuwa askari” amesema Makonda.
Makonda amezitaka mamlaka za kijeshi kuwaweka chini ya ulinzi askari hao kwa mamlaka yake ili waweze kutoa taarifa kwanini dawa za kulevya bado zinaendelea kuwepo.
Aidha, Makonda ametaja baadhi ya maeneo ambayo Wamiliki wake wamepewa vibali vya kufanya biashara lakini wanatumia maeneo hayo kinyume na masharti ya biashara kwa kuuza dawa ya kulevya ambapo amewataka kufika kituo kikuu cha polisi kesho saa tano na wasipofanya hivyo atawafata mwenyewe.