Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa atakula sahani moja na makandarasi wote waliojenga barabara chini ya kiwango jijini humo, huku akitanabaisha kuwa kwa yeyote atakuwa amejenga chini ya kiwango atafukuzwa na kulipa gharama zote za ujenzi.
Ameyasema mapema hii leo jijini Dar es salaam alipokuwa akikabidhiwa Mtaa wa Samora uliokuwa ukifanyiwa maboresho yaliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 850 uliokuwa umefadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Manispaa ya Ilala.
Amesema kuwa Jumamos hii ndio utakuwa mwisho wa makandarasi wababaisha kufanya kazi jijini Dar es salaam kwani haitaji kuona jiji kama hilo linakuwa na mashimo ambayo yaharibu taswira nzima.
“Nimeamua kuwaalika wananchi wote kwenye kongamano la jumamos ili kuweza kuelezea hali ya barabarani zilizopo mitaani kwenu, kwani wapo wakandarasi ntawafukuza siku ya jumamos, kwa hiyo siku hiyo ama mbichi ama mbivu, itajulikana siku hiyo,”amesema Makonda
Hata hivyo, ameongeza kuwa siku ya Jumamosi watakuwepo watumish kutoka Dawasco ili wajieleze kwanini mabomba yanavuja maji hovyo mitaani wakati wananchi wanasumbuka na shida ya maji.