Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imewahimiza Wasanii wa Sanaa za Ufundi wanaoishi na kufanyia kazi katika Manispaa hiyo kujisajili katika Mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi nchini (TACIP), ambao unaanza kuorodhesha wasanii kwenye Kata na Mitaa ya Kinondoni.
Wito huo umetolewa na Pilly Ngarambe kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya hiyo Desemba 14, 2018 wakati wa uzinduzi wa semina iliyo husisha Watendaji wa Kata na Mitaa katika kuutambulisha mradi wa TACIP kwao.
Pilly amesema kuwa amefurahishwa na Kampuni ya DataVision International kwa kutumia taaluma yao kuweza kuibua mradi huo na kuishirikiana na TAFCA ambao kwa pamoja wemeweza kuutekeleza kwani mradi huo unaunga mkono jitihada za Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha wajasiliamali wanatambulika na sasa wasanii ili kuwaletea maendeleo na kufika Uchumi wa Kati.
Hivyo, amewataka wasanii wote ambao wapo katika Halmashauri ya Kinondoni wajitokeze wote ili kujisajili katika mradi wa TACIP na kuwa miongoni mwa wafaidika.
Akizungumzia faida za Mradi huo, Mtaalamu wa TEHAMA kutoka Kampuni ya Datavizion International ambao ndiyo wagunduzi wa mradi huo, Dkt, Shaban Kiwanga amesema kuwa TACIP ni mradi unaokuja na manufaa mengi sana, ambapo moja ya fadia kubwa ni msanii kuweza kutambulika, kwa kuwa na kitambulisho ambacho ni cha kisasa ambacho kitamtambulisha lakini pia kitatumika kama kadi ya malipo.
Amesema kuwa kitambulisho hicho pia kitamwezesha msanii kupata mikopo kutoka katika benki na mashirika mbali mbali.
Naye, Mshauri Elekezi wa TEHAMA katika Mradi huo, kutoka Kampuni ya DataVision International, Profesa Fredrick Mtenzi amesema kuwa moja ya sababu ya TACIP kuanza usajili wa mtaa kwa mtaa katika Halimshauri ya Kinondoni ni uwepo wa wasanii wengi ambao wapo katika sanaa kwa muda mrefu, pia itatoa picha ya sehemu nyingine nyingi ambazo zitafikiwa na Mradi huo.
Na kwa upande wa Katibu wa Baraza la Sanaa Tanzia (BASATA), Godfrey Mungereza, akiwa mmoja wa wahamasishaji na watoa mada kwa watendaji amesema kuwa muda wa hadhi ya wasanii wa sanaa za ufundi kupanda umefika na yeye akiwa miongoni mwa wasanii hao tayari amesha jiandikisha TACIP na kuona faida zake.
“Pamoja na kwamba mimi ni kiongozi na nikuvua uongozi wangu, mimi ni msanii, na nikweli kwamba TACIP inakuja kuboresha hadhi ya wasanii kwani inakuja kututambulisha, na tukisha tambulika tunanufaika na kufanya kazi zetu kwa kujiamini bila kuhofia ugumu wa maisha tena” Amesema Mngereza.
Nao watendaji Kata na Wilaya wameupokea kwa furaha mradi huo na kutoa wito kwa wasanii kujitokez kwa wingi kujisajili katika mitaa yao. “Mradi huu ni mzuri na utakuwa na manufaa kwa wananchi wetu hivyo ni vyema wakajitokeza kwa wingi kujisajili” ameongeza Frola Mazengo afisa mtendaji Kata ya Kinondoni.
Katika semina hiyo Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo iliwakilishwa na Habibu Msami ambaye amewataka wasanii wa sanaa za ufundi kujithamini na kujua wanafani nzuri yenye tija ulimwenguni hivyo niwakati wao kutambulika rasmi kwa vitambulisho vya TACIP.
Aidha, baadhi ya wasanii ambao wamesha anza kunufaika na mradi huo wakitoa ushuhuda mbele ya viongozi wa Serikali Manispaa ya Kinondoni wamesema kuwa wakiwa na vitambulisho hawasumbuliwi tena na kukamatwa kwa kukosa vibai.
TACIP ni mradi wa Utambuzi wa Wasanii wa Sanaa za Ufundi nchini ambao umeibuliwa na Kampuni ya Kizawa inayojihusisha na mambo ya TEHAMA, Tafiti na Mafunzo, DataVisional International ambapo wanatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA).
Aidha mradi huo wenye baraka zote kutoka Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, mlezi wake ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Mradi huo wa kihistoria umeibuliwa nchini baada ya kutambua kuwa sanaa ya ufundi ni sanaa kongwe nchini na duniani kote, lakini imekuwa haitambuliki kutokana na shughuli zake kuendeshwa bila mpangilio rasmi.