Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Rogers Siyanga amewaomba viongozi wa dini kuiunga mkono mamlaka hiyo kwa sababu inafanya kazi kubwa ambayo inahitaji msaada wa watu wote.
Kamishna Sianga amesema hayo leo Aprili 24, 2017 katika ufunguzi wa kongamano kuhusu mmomonyoko wa maadili na athari za dawa za kulevya lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, lililofanyika mjini Dar es Salaam.
Akifungua kongamano Waziri Mkuu, Kassim majaliwa amewaomba viongozi wa dini nchini kutumia nafasi zao kuhimiza wazazi na walezi kuishi maisha yenye nidhamu, kuthamini kazi yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu na kusimamia malezi ya watoto na kuzingatia maadili ya Taifa kwa ujumla.
“Tabia na mwenendo mzuri ni lazima uanzie katika ngazi ya familia, mtaani na hatimaye katika jamii. Tukirudia utamaduni wetu wa zamani wa kusimamia maadili kwa pamoja, jamii yetu itanusurika kwa kiwango kikubwa,” amesema Majaliwa.